Kibabii University

Noah Munda Majele

Noah Munda Majele

Nilihitimu hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Kibabii na Shahada ya Uzamili katika Elimu ya Kiswahili.  Masomo katika chuo cha Kibabii yalikuwa ya kuvutia na yenye athari chanya kwani, nilipata ufahamu kamili wa nyenzo za ujifunzaji na umuhimu wake katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji darasani.

Safari hii ya kitaaluma ilisheheni mihadhara yenye kuvutia, fursa za utafiti na miradi ya ushirikiano katika ufundishaji na ujifunzaji, hali iliyoniongezea ufanisi katika lugha na ujuzi wa kufundisha. Kuanzia kwa Idara mpaka kwa Kitivo, wahadhiri walikuwa muhimu katika kubuni harakati za kitaaluma na kunipa mwongozo ambao ulivunja mipaka ya darasani, hivyo kufikia umantiki na uhalisia wa maisha ya kawaida.

Kama mzamili mahiri katika Idara ya Kiswahili, nilishiriki katika makongamano, warsha na matukio ya kitamaduni ambayo yaliimarisha uhusiano kati yangu, wanafunzi wenzangu na wahadhiri. Uzoefu huu haukukuza tu maarifa ya kitaaluma, bali pia uliniruhusu kuchangia kikamilifu katika falsafa ya Chuo.

Zaidi ya kuimarishwa kitaaluma, Chuo Kikuu cha Kibabii kilinipa mazingira yaliyonikuza kibinafsi. Kuanzisha mawasiliano na wanafunzi wenzangu na wahadhiri kuliwezesha uhusiano wa thamani katika safari ya kitaaluma. Azma ya chuo kikuu katika maendeleo kamili ilihakikisha kwamba nimetokea si tu kama mtaalamu wa Kiswahili, bali pia kama Mwalimu aliyeandaliwa vyema kwa ajili ya kukabiliana na changamoto katika sekta ya elimu.

Masomo ya shahada za upeo katika Chuo Kikuu cha Kibabii yalinijengea ujuzi wa kukuza elimu ya Kiswahili kwa kuihusisha lugha na fasihi inayovuka mipaka ya darasani. Kama mzamili, ninaendelea kushirikiana na wenzangu kupitia kwa mazungumzo, warsha na miradi inayolenga kuendeleza elimu ya Kiswahili.

Kwa ujumla, masomo ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Kibabii yalichochea ukuaji wangu kitaaluma na kibinafsi, ukaniijengea maarifa mapana katika elimu ya Kiswahili. Maarifa niliyoyapata wakati wa uzamili yatakuwa muhimu katika safari yangu ya kitaaluma ninapondelea na masomo ya uzamifu. Ni fahari kubwa na najivunia kuwa mmoja wa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kibabii.

Share on facebook
Share on twitter
Share on linkedin
Share on whatsapp