Kibabii University

Namwomboleza Profesa Ken Walibora: Jagina wa Fasihi ya Kiswahili

Namwomboleza Profesa Ken Walibora: Jagina wa Fasihi ya Kiswahili
Mwandishi: Profesa Isaac Ipara Odeo, Makamu Mkuu wa Chuo, Chuo Kikuu cha Kibabii

Prof. Ken Walibora aliyeaga dunia juma lililopita alikuwa mmoja wa majagina wa Kiswahili. Alitoa mchango mkubwa katika kukuza Kiswahili na fasihi yake unaoweza kufananishwa tu na ule wa mahashumu kama marehemu Shaban Robert au Euphrase Kezilahabi.

Jumatano tarehe 15 Mechi mwaka 2020 mwendo wa   saa mbili na dakika 39 asubuhi nilisoma taarifa kwenye mtandao iliyokanusha uvumi  kuhusu kifo cha Ken Walibora, ukiutaja kuwa  porojo. Aliyetuma ujumbe huo alidai kuwa hiyo ilikuwa  mara ya pili ya habari za kupotosha kama hizo kusambazwa. Dakika moja baada ya tukio hilo, nilipiga simu ya Profesa Walibora lakini haikuingia. Hapo ndipo nilipompigia mwendani wake Masinde Kusimba aliyekiri kupokea taarifa kuhusu kifo cha Walibora ila hakuwa amethibitisha. Ukweli ulithibitishwa kwangu na Carol Weloba, aliyekuwa zamani mhariri wa Kiswahili Shirika la Oxford saa 10:22, kwa sauti ya kitetemeko na  huzuni.

Itakuwaje mtu maarufu kama huyu kifo chake kitokee kwa namna hiyo? Katika vitabu vyake vingi alizungumzia kifo. Je ilikuwa sadfa? Nilijiuliza. Prof. Walibora alikuwa mtangazaji maarufu na baadaye akawa mwalimu na mwandishi mtajika wa Kiswahili na fasihi nchini , ukanda wa Afrika Mashariki, Afrika na Dunia nzima.

Nililisikia jina la Ken Walibora kama msanii mara ya kwanza mwaka 1997. Nilikuwa mwanachama wa jopo la Kiswahili sekondari katika Taasisi ya Ukuzaji Mitaala ya Kenya.  Mwaka huo nilishiriki zoezi la kutathmini vitabu viteule vya kuidhinishwa kwa ajili ya mafunzo ya fasihi katika shule za sekondari. Nakumbuka nilitetea vikali kupendekezwa kwa riwaya yake ya Siku Njema. Awali nilikuwa namfahamu Walibora kama mwanahabari niliyemwona tu kwenye televisheni.

Niilikutana naye ana kwa ana mwaka 1999 katika Taasisi iyo hiyo. Wakati huu kwenye warsha ambapo aliwasilisha makala kuhusu “Fumbo la Kitumbua Kimeingia Mchanga.”

Nilipata nafasi ya kutalii baadhi ya maandishi yake kuanzia mwaka 2003. Kama mwandishi wa Ijaribu na Uikarabati nilizihakiki na kuzitungia maswali ya marudio na majibu kazi zake kama vile riwaya ya Kidagaa Kimemwozea, na hadithi fupi ya “Tuzo” katika mkusanyiko wa hadithi wa Mayai Waziri wa Maradhi na “Damu Nyeusi” kwenye diwani ya anwani hiyohiyo. Huu ulinipa msukumo wa kusoma kazi zake nyingine kama vile Nasikia Sauti ya Mama. Niliweza kumwelewa mwandishi Walibora zaidi. Katika uandishi wake alielekezwa na falsafa ya udhanaishi huku mtindo wake wa kuandika ukikaribiana na ule wa Shabaan Robert. Kazi zake zilielekezwa na motif ya safari. Alitetea utu, wema na maisha bora kama lilivyodokeza jina lake. Katika kazi zake alikemea ukengeushi, usaliti na udhalimu kati ya maovu mengine.

Tuliaanza kutangamana kwa karibu aliporejea kutoka Marekani baada ya kuhitimu shahada ya Uzamifu. Tulikutana  katika makongamano mbalimbali humu nchini na nje. Mimi na wapenzi wengine wa Kiswahili tulishangilia alipopewa wadhifa wa Meneja wa Ubora katika Shirika la Nation. Tulijua kuwa yeye angedumisha matumizi sahihi ya lugha kwa kuwa vyombo vya habari vimelaumiwa kwa kuchangia matumizi mabaya ya lugha ya Kiswahili.

Kilele cha mahusiano yangu na Walibora ni tarehe 27 Novemba 2015 alipowasilisha mhadhara mzito katika Chuo Kikuu cha Kibabii. Hatimaye alikubali kuwa mhadhiri wa muda katika chuo hiki. Wanafunzi wake wa shahada ya kwanza na uzamili hawatasahau kamwe uelekezi na malezi yake ya kitaaluma.

Wanaomfahamu Profesa Ken Walibora kwa karibu wanamkumbuka kwa mambo manne: Awali ya yote, alikuwa mpenzi wa Kiswahili, lugha aliyoienzi kwa dhati. Kwa sauti laini lakini iliyoficha makali, aliwakemea wote waliokidunisha Kiswahili huku akiwahimiza wenyeji wa Ukanda wa Afrika Mashariki kuwa Kiswahili kitakwezwa tu kupitia ari na juhudi za wasemaji wake.

Pili ni mhalaka wake kama mtu mcheshi, mpole, mnyenyekevu, na aliyemjali na kumsikiza kila mtoa hoja awe mdogo au mkubwa, tena kwa makini.

Tatu, ilikuwa kipawa chake cha uzito wa mawazo na uwezo wa kuhakiki na kutoa hoja kwa mantiki na muwala wa kupendeza.

Jambo la nne lilikuwa sauti yake nyororo na ya kuongoa ambayo kwa sikio kali ilisikika kidogo kama iliyokuwa na mwangwi!

Mwezi wa Mechi mwaka huu wa 2020, nilimwomba aupitie mswada wa kazi kuhusu maisha yangu na akakubali na kuikamilisha kwa muda wa wiki mbili. Tuliwasiliana naye mwisho wa mwezi uo huo kuhusu kitabu ambacho yeye na Masinde Kusimba walikuwa wanaandika juu ya maisha ya Leornard Mambo Mbotela.

Alikuwa ameahidi kuandika blabu ya kitabu changu, ila ilibidi aitikie wito wa Muumba wake. Tunamtakia buriani kurudi Cherenganyi, Trans Nzoia. Mungu aifariji familia na marafiki zake na ailaze roho yake mahali pema hadi tutakapokutana.

 

Profesa Isaac Ipara Odeo, Makamu Mkuu wa Chuo, Chuo Kikuu cha Kibabii 0725429397; iodeo@kibu.ac.ke

Share on facebook
Share on twitter
Share on linkedin
Share on whatsapp