Mimi ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kibabii, Mwaka wa 2025, nikiwa nimehitimu Shahada ya Uzamifu (PhD) katika Masomo ya Kiswahili wakati wa Mahafali ya 10 ya Chuo yaliyofanyika Ijumaa, tarehe 21 Novemba 2025. Tasnifu yangu ya Uzamifu yenye mada: Uongozi na Uafikiaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (Leadership and the Realisation of Sustainable Development Goals) ndiyo hitimisho la safari niliyoianza mwaka 2021, muda mfupi baada ya janga la UVIKO-19. Maisha ni safari. Safari yangu ya elimu ilianza katika mazingira magumu yaliyokaribia kuninyima fursa ya kujiunga na shule ya upili. Kupitia msaada wa wazazi wangu marehemu, niliweza kujiunga na shule ya kutwa, hatua iliyochochea azma yangu ya kufanikiwa kielimu.
Mwaka wa 2010, niliingia Chuo Kikuu cha Egerton, Behewa la Laikipia kusomea Shahada ya Elimu (Sanaa), ambapo nilihitimu kwa Heshima ya Daraja la Kwanza (1 st Class Honors) na kutunukiwa tuzo ya mwanafunzi bora katika Kitivo cha Elimu. Mnamo 2013, niliendelea na masomo ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Maseno na kuhitimu Shahada ya Uzamili katika Kiswahili mwaka 2019. Taasisi hizi mbili zilijenga msingi imara wa kitaaluma ninaouenzi sana.
Hamu ya kusomea Uzamifu ilikuwa ya muda mrefu, ijapokuwa sikuwazia awali kujiunga na Chuo Kikuu cha Kibabii. Namshukuru Dkt. Robert Kati, Mtiva wa Shule ya Upeo, na Dkt. Fred Simiyu wa Idara ya Kiswahili na Lugha Nyingine za Kiafrika kwa kunihimiza kujiunga, uamuzi ambao sijawahi kuujutia. Kibabii ilinipokea katika idara iliyojaa uimara, ushirikiano na kujitolea, chini ya uongozi wa mshikilizi wa Idara, Dkt. Gladys Kinara. Najivunia kuwa sehemu ya kizazi cha kwanza cha wanadokezi 11 wa PhD katika Masomo ya Kiswahili, ambapo wanne tulihitimu mwaka 2025. Ninathamini kwa dhati ushirikiano, mshikamano na umoja wa kitaaluma tulioujenga, kundi hili likiongozwa na Dkt. Stephen Ndinyo Muyundo.
Katika mwaka wangu wa kwanza wa masomo ya Uzamifu, nilikabiliana na changamoto ya kumtunza mama yangu aliyekuwa akiugua huku nikijaribu kusawazisha majukumu ya kazi, huduma za kichungaji na masomo mazito. Kifo chake kabla ya mitihani ya muhula wa pili kilijaribu ustahimilivu wangu kwa kiwango kikubwa, lakini Idara ya Kiswahili, wenzangu darasani na jamii ya Chuo kwa ujumla ilinipa faraja na msaada uliorahisisha kipindi cha uponyaji na ustahimilivu.
Nawashukuru kwa udhati wa moyo wasimamizi wangu—Prof. Isaac Ipara Odeo na Dkt. Deborah Nanyama Amukowa—kwa mwongozo na msaada wao wa hali na mali katika kila hatua. Vilevile, naitambua na kuithamini familia yangu, hususan mke wangu, Bi. Maureen Juma, na watoto wetu kwa upendo na usaidizi wao usiokatika wakati wote wa safari hii.
Kupitia safari hii, nimejifunza kwamba hakuna lisilowezekana. Kama asemavyo Wayne Gerard Trotman, “Mambo mengi huonekana kuwa magumu hadi pale unapojaribu.” Nakienzi Chuo Kikuu cha Kibabii kwa kugeuza ndoto iliyowahi kuonekana kuwa ngumu kuwa tukio la kihalisia. Bila shaka, ni taasisi inayojulikana kwa kujitolea, ufanisi na huduma bora yenye mifumo thabiti.
Kibabii, Hoyeee!