Kati ya nchi zilizoshuhudia maendeleo makubwa ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiteknolojia ni zile za bara Asia zikiwemo Japani, Malaysia na Korea Kusini. Uchumi wa nchi hizi sasa hivi unatishia ule wa miamba kama Amerika, Ujerumani na nchi nyingine zilizoendelea kiuchumi. Vyuo vikuu vyao ni kati ya vile ambavyo huchukua nafasi za mbele katika orodha ya vyuo vikuu bora duniani. Nchi hizi zilikuwa katika kiwango sawa cha maendeleo na Kenya na nchi jirani katika ukanda wa Afrika Mashariki miaka ya 1965 hadi 1970. Sababu kubwa ya maendeleo haya ya haraka si utamaduni tu bali ni uanuai wa utamaduni wao. Yaani uwezo wa kukopa sifa za tamaduni mbalimbali ili kuimarisha wao.
Tamaduni za nchi hizi zimeweka msingi wa kimaadili ambao umewapa raia msukumo wa kuwajibika katika utendaji kazi. Mfano wa uwajibikaji ulioshuhudiwa hivi majuzi huko Uchina (ingawa unahitaji ithibati) ni kukarabatiwa na kuzinduliwa kwa hospitali inayolazwa wagonjwa elfu moja katika muda wa siku tisa tu!
Hata sisi Waafrika tumekuwa na utamaduni wetu tangu jadi. Tatizo ni kuwa tumeshindwa kuutumia utamaduni huu kuchapuza maendeleo ya jamii. Kwa bahati mbaya, kushindwa huku kumechangiwa pakubwa na tabia ya kudharau vya asili na kukimbilia vya wageni kutokana na imani potofu kuwa ndivyo bora ingawa ni bayana kuwa Afrika ina utajiri mkubwa kitamaduni.
Mhimili wa dhana ya utamaduni ni mila na desturi. Ndio maana kuna methali za Kiafrika kama: Mkataa kwao ni mtumwa, Mwacha mila ni mtumwa, Mwacha asili ni mtumwa na Mwacha kwao ni mwasi, endako hana kiasi.
Lakini utamagduni ni nini? Kuna vijelezi vingi vya neno hili lakini hapa tutajifunga kwenye maelezo kuwa utamaduni ni mwenendo, mfumo, mtazamo au utaratibu wa watu wa kuendesha maisha yao unaowatofautisha na wanyama na hata watu wa maeneo mengine. Kwa mfano Watanzania hujitambulisha kwa undugu, utulivu, lugha ya Kiswahili na mshikamano wao. Ni nini kinachotutambulisha sisi Wakenya.
Nguzo za utamaduni ni desturi, mila, sanaa, michezo, historia, heshima, mavazi, ujuzi, imani, sheria, fasihi, sayansi na mengineyo.
Vipengele vya msingi hata hivyo ni mila na desturi. Hivi ndivyo huhalalisha na kuharamisha matendo yote ya binadamu. Yaani huwa kama sheria inayotukuza matendo yakubalikayo na kuadhibu yale yaliyokatazwa.
Utamaduni una sifa maalumu. Katika kila jamii, utamaduni hukua, hubadilika, hurithishwa na hata hufifia. Katika utamaduni kuna mambo mazuri ya kuenzi na kuonea fahari. Kwa upande mwingine yapo yale yaliyopitwa na wakati ambayo hupigwa vita. Jamii nyingi za Kiafrika zinawaonya wanajamii wao kuepukana na ukeketaji, mapenzi ya kiholela, ulevi wa kupindukia na ndoa za wasichana wa umri mdogo kwa kuwa hayana tija.
Kwa jinsi hii, utamaduni ni jambo linalomhusu binadamu katika ngazi mbalimbali kuanzia mtu binafsi, familia, ukoo, kabila, asasi kama chuo kikuu, nchi, bara na ulimwengu mzima.
Chuo Kikuu cha Kibabii kimejenga utamaduni wake kama asasi. Utamaduni huu unajipambanua kupitia tunu zake sita ifuatavyo:
- Ubora wa hali ya juu: Unajitokeza kupitia ulimbwende katika kutenda mambo, mvuto wa majengo na mandhari ya kupendeza.
- Uwajibikaji na uwazi: Yaani hali ya kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
- Majukumu ya kijamii: Haja ya kutenda inavyopasa, kuwajali na kuwaheshimu wengine.
- Ubunifu/uvumbuzi: Daima kuweka mikakati ya kuboresha maisha ya wadau.
- Uadilifu: Kitambulisho chake ni maadili, adabu, mavazi ya kiheshima na unyenyekevu.
- Uhuru wa kitaaluma: Utoaji wa maarifa bila kudhibitiwa na hali ya kutoa maoni bila uoga.
Tunu hizi zimepewa uhai kwa kusawiriwa kwenye nembo ya Chuo Kikuu cha Kibabii iliyo hapo juu; huku kila kipengele kikiwakilisha maana maalumu.
- Ngao – ni kulinda tunu/maadili ya Chuo Kikuu.
- Tufe/mduara wa dunia – kumaanisha Kibabii ni miongoni mwa vyuo viku vingi ulimenguni.
- Ramani ya Afrika – Yaani Chuo Kikuu hiki ni moja ya asasi muhimu katika Bara la Afrika lenye matumaini.
- Mizunguko – Mshikamano wa watu wa Chuo Kikuu cha Kibabii kama familia moja inayozingatia maadili.
- Rangi ya dhahabu – Kielelezo cha hadhi, utukufu na ubora wa mitaala.
- Rangi ya samawati – Rangi ya bahari na anga inayoashiria rasilmali kubwa na azma ya Chuo Kikuu kutimiza makuu.
- Tepe – Kiwakilishi cha ubunifu thabiti usio na kikomo.
- Nyota – Ishara ya matarajio makubwa ya Chuo Kikuu cha Kibabii.
- Rangi nyeupe – Usafi wa nia na uwazi wa azma.
Hatuna budi kuukumbatia, kuushangilia na kuudumisha utamaduni wa Chuo Kikuu cha Kibabii kwa kuelekezwa na tunu zilizo hapo juu kwa ajili ya kujenga asasi itakayochangia ustawi wa jamii na taifa la Kenya sasa na katika mustakabali.