Off Bungoma-Chwele Road
sgs@kibu.ac.ke
+254721589365
Dr. Robert Kati
Office Hours: Monday–Friday
8:00 AM – 5:00 PM
sgs@kibu.ac.ke
Dr. Robert Kati
8:00 AM – 5:00 PM
Fasihi kama kioo cha jamii inachangia katika maendeleo na masuala ibuka ya jamii yakiwemo yale ya uongozi. Fasihi inaweza kushirikishwa katika kuafikia mpango wa kimaendeleo wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (MME). Uongozi ni suala muhimu katika jamii na hudhihirika kupitia mikakati kadhaa, mojawapo ukiwa utekelezaji wa MME. Mpango huu hauwezi kuafikiwa bila uongozi bora katika mataifa ya ulimwengu. Umoja wa Mataifa (UM) unatambua umuhimu wa uongozi na ushirikano katika kufanikisha uafikiaji wa MME. Mpango wa MME umekumbatiwa na wasomi, wataalamu, mashirika na serikali mbalimbali duniani kwa kuwa ni njia ya kuafikia maendeleo. Waandishi wa fasihi wameshughulikia masuala ya uongozi na maendeleo katika kazi zao. Kuna tafiti zilizoangazia suala la uongozi katika fasihi. Nyingi yazo zimeangazia namna uongozi unavyojitokeza katika fasihi bila kuhusisha MME. Utafiti huu ulilenga kuchunguza uongozi na uafikiaji wa MME katika tamthilia teule za Kiswahili. Utafiti uliongozwa na madhumuni mahsusi yafuatayo: kudadavua aina za uongozi katika tamthilia teule za Kiswahili; kupambanua MME yanayojitokeza katika tamthilia teule za Kiswahili; kutathmini mikakati waliyotumia viongozi kukabiliana na changamoto zinazokumba uafikiaji wa MME katika tamthilia teule za Kiswahili. Nadharia ya Uhistoria Mpya iliyoasisiwa na Stephen Greenblatt (1980) na kuendelezwa na Brizee na Tompkins (2012) ilitumika. Muundo wa kiuchanganuzi ulitumiwa. Utafiti uliangazia tamthilia zilizotungwa kuanzia mwaka wa 2016 hadi mwaka 2024 kwa kuwa ndicho kipindi cha utekelezaji wa MME. Kwa kutumia mbinu ya usampulishaji dhamirifu, tamthilia nne ziliteuliwa. Hizi ni: Shamba la Halaiki (Okello, 2016), Mwinyi na Manyani ya Adili (Mbogo, 2022), Kifunganjia (Okello, 2021) na Kodi (Muhando, 2024). Data ilikusanywa kupitia mbinu ya unukuzi. Tamthilia teule zilisomwa na data kuibuliwa kwa usaidizi wa orodha ya uthibitishaji. Aidha, kupitia dodoso, utafiti uliwahoji waandishi wa tamthilia teule. Data hii ilipangwa kisha kuchanganuliwa kwa njia ya uhakiki wa yaliyomo. Matokeo yaliwasilishwa kwa njia ya maelezo. Utafiti huu umebaini kuwa fasihi hususan tamthilia, ni nyenzo muhimu katika kuchangia uafikiaji wa MME. Matokeo yanaonyesha kuwa uongozi bora ni nguzo muhimu ya uafikiaji wa MME. Vilevile, imebainika kuwa kilimo ni miongoni mwa mikakati inayoweza kutumiwa na viongozi kama njia madhubuti ya kufanikisha malengo hayo. Utafiti huenda ukatoa mwanga kwa viongozi mbalimbali kuhusisha fasihi katika kuratibu na kupanga mipango ya utekelezaji wa MME. Utafiti unapendekeza kuwa viongozi waendeleze uongozi mzuri kwani unachangia maendeleo. Mwisho, wahimize wananchi kuzidisha juhudi katika sekta ya kilimo kwa kuwa kilimo kitachangia uafikaji wa malengo kadhaa ya mpango MME.