Off Bungoma-Chwele Road

sgs@kibu.ac.ke

+254721589365

Prof. Robert Kati

Office Hours: Monday–Friday

8:00 AM – 5:00 PM

Uchawi Na Utekelezaji Wa Malengo Ya Elimu Na Kiswahili Nchini Kenya: Mfano Wa Hadithi Fupi Teule

Student’s Name:
Shikanda Paul Kaggwa Andrew

Supervisors:
1.Dkt. Wanjala Fred Simiyu
2. Dkt. Simiyu Benson Sululu

Master Of Education In Kiswahili

ABSTRACT

Utafiti huu ulihusu aina za uchawi na taashira zake katika utekelezaji wa malengo ya elimu nchini Kenya, kwa kutumia hadithi fupi teule za Kiswahili zinazotumiwa katika Shule za upili nchini Kenya. Malengo mahsusi ya utafiti huu yalikuwa: kubainisha aina za uchawi unaojitokeza katika hadithi fupi teule. Kuchunguza taashira za kiuchawi katika hadithi fupi teule za Kiswahili ili kutekeleza malengo ya elimu nchini Kenya. Tatu, kudadavua jinsi ambavyo aina na taashira za uchawi zinavyotumika kutekeleza malengo ya elimu nchini Kenya. Utafiti ulitumia maudhui ya uchawi, matukio na mandhari katika hadithi fupi teule za Kiswahili. Hadithi fupi teule zilikuwa kama jukwaa la kujadili aina za uchawi na taashira zake katika utekelezaji wa malengo ya elimu nchini Kenya. Utafiti huu ulijikita kwa malengo mawili, kati ya malengo manane ya elimu nchini Kenya. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya uchawi iliyoasisiwa na Pritchard (1937). Utafiti ulijikita kwa mihimili ya nadharia ya uchawi minne. Mhimili wa kwanza unaeleza kuwa kuna uchawi unaosababisha kuwapo utengano baina ya wanajamii. Mhimili wa pili nao unabaini kuwepo nguvu za kuvuta au kusambaratisha mapenzi. Mhimili wa tatu unadai kuwepo uchawi wa mazingaombwe. Mhimili wa nne unaeleza kuwepo kwa utoaji wa kafara katika jamii. Nadharia ya uchawi ilimfaa mtafiti kwa uchawi na taashira zake zinavyoweza kuendeleza maadili katika jamii na athari zakumuongoza katika ukusanyaji, uchanganuzi na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti. Utafiti huu ulitumia malengo manane ya elimu nchini Kenya na kuegemea kwa malengo mawili, lengo la nne la kuendeleza uadilifu na amali za kidini na lengo la sita la kukuza, kuhifadhi na kuthamini tamaduni za jamii mbalimbali. Utafiti huu ulifanyiwa maktabani. Mtafiti alitumia mbinu ya kuchanganua yaliyomo na upekuzi wa nyaraka ili kupata data, hasa kutoka hadithi fupi teule za Kiswahili, vitabu, tasnifu na majarida yenye vianzo vilivyo na uhusiano na mada ya utafiti. Utafiti ulitumia mbinu ya usampulishaji makusudi ili kupata sampuli tano za hadithi fupi teule za Kiswahili kutoka diwani tano za hadithi fupi za Kiswahili. Matokeo ya utafiti yalibainisha aina tofauti za uchawi katika hadithi fupi teule, taashira za uchawi katika kuendeleza malengo ya elimu nchini na athari za aina ya uchawi katika kutekeleza malengo hayo’. Matokeo ya utafiti huu yalidhibitisha kuwa maudhui ya uchawi yamejitokeza katika kazi za fasihi andishi katika vitabu vya kiada na ziada vinavyotumika katika shule za upili. Matokeo ya utafiti huu yanatarajiwa kuwanufaisha wanafunzi, walimu na wakuza mitaala kuwa maudhui ya uchawi yanaweza kutumika kutekeleza malengo ya elimu kwa kurejelea hadithi fupi teule za kufunza kiswahili. Utafiti huu kwa ujumla unatarajiwa kutimiza uelewaji wa aina na taashira za uchawi katika utekelezaji wa malengo ya elimu nchini Kenya.